Rais Rouhani: Kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi hakuhitajii vikosi vya kigeni
(last modified Wed, 14 Aug 2019 12:51:43 GMT )
Aug 14, 2019 12:51 UTC
  • Rais Rouhani: Kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi hakuhitajii vikosi vya kigeni

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, ili kudhamini usalama na utulivu katika Ghuba ya Uajemi hakuna haja ya kuweko vikosi vya kieneo katika eneo hilo.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri na kubainisha kwamba, nchi za eneo zinaweza kulinda usalama wao kwa kudumisha umoja, mshikamano na mazungumzo baina yao.

Rais Rouhani ameeleza kuwa, nara zote zinazotolewa kuhusiana na kuundwa muungano mpya katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ni za kidhahiri tu na zisizoweza kutekelezwa kivitendo.

Rais wa Iran amesema, malengo ya hatua za madola makubwa hususan Marekani katika eneo hili, hayana kingine ghairi ya kuzusha mifarakano na kuzifanya kuwa tupu hazina za nchi za Kiislamu katika eneo.

Rais Hassan Rouhanii wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Kadhalika Rais Rouhani amezungumzia mpango wa utawala haramu wa Israel unaodai kwamba, unataka uwepo katika usalama wa eneo na kusema kuwa, Wazayuni kama wanaweza basi na wajidhaminie usalama wao.

Aidha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba, chimbuko kuu la ugaidi, vita na mauaji katika eneo hili la Mashariki ya Kati ni utawala ghasibu wa Israel.

Rais Rouhani amezungumzia pia kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hatua ya madola ya Ulaya ya kutotekeleza ahadi zao na kusema kuwa, baada ya kumalizika siku 60 muda ambao Iran imeyapatia madola hayo, Tehran itaingia hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Tags