Brigedia Jenerali Baqeri: Iran imebadilisha vikwazo kuwa fursa ya kujiimarisha
Mkuu wa Kamandi Kuu ya Majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria vikwazo vya kidhalimu vya maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa: "Iran imebadilisha vikwazo kuwa fursa ya kustawi kuelekea katika nguvu na uwezo mkubwa."
Brigedia Jenerali Muhammad Baqeri Mkuu wa Kamandi ya Majeshi yote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo Jumamosi alipotembelea Shirika la Viwanda vya Anga katika Wizara ya Ulinzi ya Iran mjini Tehran na kuongeza kuwa: "Hatua za kijihadi za wataalamu Wairani katika kuboresha sekta ya viwanda vya ulinzi ni utekelezaji kivitendo wa nara ya 'sisi tunaweza." Aidha amesema njia hii ya kuelekea katika izza na heshima ilianza kwa utengenezaji wa vipuri vichache na leo imefika katika kiwango cha uundwaji injini za kisasa za ndege na helikopta.
Brigedia Jenerali Baqeri ameendelea kusema kuwa, kuimarisha uwezo wa kujihami na kumzuia adui katika hali ambayo Iran inakabiliwa na vikwazo kutawezekana tu kwa kujizalishia zana za kivita ndani ya nchi kwa kutegemea wasomi vijana.
Mkuu wa Kamandi Kuu ya Majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia kutunguliwa ndege isiyo na rubani ya Marekani au drone ya kijasusi na ya kisasa kabisa ya Marekani kwa kutegemea mfumo wa kujihami angani uliotengenezwa kikamilifu nchini Iran na kusema hiyo ni hatua muhimu na kubwa sana.
Amesema hatua hiyo yenye thamani kubwa iliishangaza dunia nzima zikiwemo nchi ambazo zinaongoza katika uga wa mifumo ya kujihami angani.
Ikumbukwe kuwa mnamo Juni 20 mwaka huu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilitungua drone ya kijasusi ya Marekani ya Global Hawk ambayo ilikuwa imekiuka anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.