Zarif: Iran haina hamu ya kufanya mazungumzo na serikali ya Washington
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Tehran haina hamu ya kufanya mazungumzo na Washington na upatanishi wa aina yoyote ule baina ya pande mbili unapaswa kujikita katika suala la kuirejesha Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Akizungumza na waandishi habari akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland huko Helsinki, Muhammad Javad Zarif amesema kuwa, Marekani inapaswa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama lililotolewa tarehe 20 Julai mwaka 2015 lilifuta maazimio yote 6 ya kabla yake ya baraza hilo dhidi ya Iran ambayo yalipelekea kuwekewa vikwzo Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na kadhia ya nyuklia.
Katika upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa hatua ya utawala wa eneo la Jabal Tariq (Gibraltar) ya kukamata meli ya mafuta ya Iran kwa amri ya Uingereza na Marekani ilikuwa kinyume cha sheria.
Ameeleza kuridhishwa kwake na uamuzi wa kuiachia meli hiyo na kusema: Hukumu ya mahakama ya Marekani na kusimamishwa tena meli hiyo ya Iran imetolewa kwa matashi na malengo ya kisiasa.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Pekka Haavisto amesema nchi yake ni muungaji mkono mkubwa wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.