Iran, mdhamini wa usalama wa Lango Bahari la Hormuz
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55510-iran_mdhamini_wa_usalama_wa_lango_bahari_la_hormuz
"Kupita kwenye Lango Bahari la Hormuz ni huru kwa wote na Iran inadhamini usalama wa lango bahari hilo".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 21, 2019 07:56 UTC
  • Iran, mdhamini wa usalama wa Lango Bahari la Hormuz

"Kupita kwenye Lango Bahari la Hormuz ni huru kwa wote na Iran inadhamini usalama wa lango bahari hilo".

Hayo yameelezwa na kamanda wa kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Admeri Alireza Tangsiri wakati alipotembelea sekta ya ufundi ya zana za baharini ya Wizara ya Ulinzi ya Iran mjini Bandar Abbas, kusini mwa nchi.

Admeri Tangsiri ameeleza bayana kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasimama imara kukabiliana na nchi za nje ya eneo hili na maajinabi ambao wanajiingiza kwenye Ghuba ya Uajemi kwa madhumuni ya kutoa vitisho, kuvuruga amani na kuzusha machafuko; na itatekeleza jukumu lake la kuhakikisha amani inakuwepo katika eneo hilo.

Admeri Alireza Tangsiri

Usalama wa Lango Bahari la Hormuz  na Ghuba ya Uajemi vina umuhimu wa kistratejia katika mlingano wa kiusalama kimataifa na kieneo, na ndio maana hatua yoyote ya kujaribu kuvuruga usalama huo haiwezi kufumbiwa macho.

Kutokana na stratejia yake ya kiusalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi inayotilia mkazo usalama jumuishi wa nchi zote za eneo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga uingiliaji wa aina yoyote ile wa maajinabi katika masuala ya usalama ya eneo hili. Halikadhalika inaziasa nchi zote jirani za kusini mwa Ghuba ya Uajemi ziachene na mitazamo ya kukabidhi hatamu za kudhamini usalama wa eneo kwa maajinabi na chokochoko cha kuzusha mivutano; na badala yake kuishi kwa maelewano na ujirani mwema.

Kuhusiana na nukta hiyo, mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa Majid Takht-Ravanchi amesema, kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi ni jukumu la nchi za pwani hiyo; na akafafanua kwamba: Uwepo na uingiliaji wa vikosi vya majeshi ya kigeni katika njia hiyo ya majini ya kistratejia, kunavuruga uthabiti na hakukubaliki.

Majid Takht Ravanchi, mwakilishi wa Iran UN

Ravanchi ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kujadili changamoto za amani na usalama katika Mashariki ya Kati na akasisitiza kwamba, jaribio lolote la kuanzisha miungano bandia ya kulinda usalama wa vyombo vya majini katika eneo la Ghuba ya Uajemi litafeli na kugonga mwamba.

Kukabidhi hatamu za kudhamini usalama wa eneo kwa majinabi kunakofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi ni sawa na kukaribisha uingiliaji wa madola ya nje ya eneo hili. Marekani imetumia visingizio viwili vya usalama na uchumi kuhalalisha uingiliaji wake katika eneo. Kisingizio cha usalama cha mpango huo kimelenga uthabiti na usalama wa vyombo vya majini katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz.

Mkakati wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na masuala yote hayo mawili ni kusimama imara kukabiliana na mashinikizo ya Marekani. Sera inazotekeleza Iran kuhusiana na usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz zimejengeka juu ya msingi wa kumfanya adui asithubutu kuanzisha hujuma na vile vile kuzuia vitisho. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeratibu uwezo wake wa kiulinzi na kiusalama kulingana na vitisho vinavyoikabili kwa kufuata usuli, kanuni na sheria za kimataifa. Kwa hivyo uanzishaji wa miungano bandia ya aina hiyo, endapo utahatarisha maslahi ya Iran katika eneo, bila shaka utaigharimu pakubwa Marekani, Uingereza, Bahrain, Imarati na Saudi Arabia au mwengine yeyote yule atakayejiunga na muungano huo.

Rais Hassan Rouhani (kulia) na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Katika mazungumzo ya simu ambayo Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya hivi karibuni na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, alimueleza kiongozi mwenzake huyo kwamba, siasa za Marekani za kuzusha mivutano katika eneo zina taathira hasi kwa amani na uthabiti wa nje ya eneo na kimataifa. Dakta Rouhani alisisitiza kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa na itaendelea kuwa mdhamini mkuu wa usalama na uhuru wa safari za vyombo vya majini katika eneo la Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormuz na Bahari ya Oman.

Abdel Bari Atwan, mchambuzi mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiarabu anaizungumzia hatua ya Marekani ya kuanzisha muungano wa baharini katika Ghuba ya Uajemi kwa kusema: Kinyume na wanavyodhani viongozi wa Waarabu, inavyoonekana, Marekani na Wazayuni wamezungumzia utayari wa Tel Aviv wa kujiingiza Ghuba ya Uajemi, ili kuanzisha mchezo mpya kwa madhumuni ya kuzikamua na kuzinyonya nchi za Kiarabu.

Lakini pamoja na hayo, majibu makali na ya nguvu iliyotoa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, likiwemo la kuitungua ndege vamizi isiyo na rubani ya ujasusi ya Marekani na kuizuia meli ya mafuta ya Uingereza iliyokiuka sheria katika Ghuba ya Uajemi, yameonyesha kuwa Tehran haina mzaha na yeyote yule atakayeanzisha chokochoko za kuzusha mivutano  katika eneo hili.

Katika moja ya mahojiano aliyowahi kufanyiwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alizungumzia suala la kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi kwa kusema: "Sisi tuna mpaka wenye urefu wa maili 1,500 katika Ghuba ya Uajemi. Na hiyo ndiyo sababu ya kuitwa Ghuba ya Uajemi, si Ghuba ya Mexico, kwani iko jirani na sisi."

Ukweli ni kwamba kudhamini usalama na uhuru wa safari za vyombo vya majini ni miongoni mwa maslahi muhimu ya Iran katika uga wa usalama wake wa taifa; na bila ya Iran, hakuna yeyote awezaye kudhamini usalama wa eneo hili la majini. Hii ni maudhui iliyotiliwa mkazo pia katika mazungumzo aliyofanya Waziri Zarif katika safari yake ya kuzitembelea nchi tatu za Ulaya.../