Iran yaonyesha satalaiti, yakanusha madai ya Trump
Iran imeonyesha hadharani satalaiti yake ya mawasiliano inayojulikana kama Nahid 1 na hivyo kukanusha madai ya Rais Donald Trump wa Marekani ambaye amedai kuwa satalaiti hiyo imeanguka wakati ilipokuwa inarushwa katika anga za mbali.
Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Iran Mohammad Javad Azari Jahromi, mapema leo Jumamosi amewatembeza waandishi habari katika kituo cha utafiti wa anga za mbali na kuwaonyesha satalaiti hiyo iliyotengenezwa hapa Iran na haikuwa na sehemu yoyote iliyoharibika.
Jahromi pia ametuma picha katika akaunti yake ya Twitter akiwa pembizoni mwa satalaiti hiyo ya mawasiliano na kuandika: "Mimi hapa na Nahid 1 hivi sasa. Sabahalkheri Donald Trump!"
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Trump kueonesha katika akaunti yake ya Twitter picha ya kile alichodai ni 'ajali mbaya' katika kituo cha kutuma satalaiti katika anga za mbali katika mkoa wa Semnan kaskazini mwa Iran. Trump amedai kuwa ajali hiyo imetokea katika hatua ya mwisho ya kutumwa satalaiti hiyo ya Iran katika anga za mbali na kusema kuwa Marekani haijahusika na ajali hiyo.
Hata hivyo punde baada ya madai hayo ya Trump, Waziri Azari Jahromi alituma ujumbe katika Twitter na kusema Satalaiti ya Nahid 1 iko salama katika maabara, na waandishi habari wanakaribishwa kuitazama.
Iran imesema itarusha satalaiti tatu katika anga za mbali kabla ya kumalizika mwaka huu. Satalaiti hizo ni Nahid 1, Zafar na Pars 1.
Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa ijulikanayo kwa jina la Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009. Iran pia imetangaza kuwa, katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanaadamu katika anga za mbali. Tayari mazoezi yameshafanyika kuhusiana na lengo hilo kwa kutumwa nyani hai katika anga za mbali ambaye alirejea ardhini akiwa salama.
Mafanikio haya ya Iran yamepatikana licha ya kuwepo vikwazo vya kila upande vya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kislamu.