Sep 10, 2019 12:51 UTC
  • Iran ya Kiislamu yaghariki katika maombolezo ya Siku ya Ashura

Mamilioni ya wananchi wa Iran, leo Jumanne wameadhimisha kwa shauku na hamasa kubwa siku ya maombolezo makubwa ya Ashura, kukumbuka siku aliyouawa shahidi kidhulma Bwana wa Mashahidi, mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Husain AS katika jangwa la Karbla (la Iraq ya leo).

Ashura ni mwezi 10 Mfunguo Nne, Muharram, ambayo mwaka huu imesadifiana na leo Jumanne tarehe 10 Septemba, 2019.

Waislamu wa madhehebu, matabaka na rika mbalimbali nchini Iran wameshiriki kwa mamilioni katika kumbukumbu hizi chungu zinazokumbushia siku mjukuu huyo kipenzi, mmoja wa mabwana wa vijana  wa peponi alipouawa shahidi kikatili akiwa pamoja na masahaba wake 72, huko kusini mwa Iraq ya leo. 

Kumbukumbu ya Siku ya Ashura 1441 Hijria, Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran

 

Moja ya mafundisho muhimu sana aliyotufunza Imam Husain AS katika siku ya Ashura ni kwamba, hakuna jambo lolote linalopaswa kufanywa kisingizio cha kutosimamisha Sala kwa wakati wake. Katika mazingira magumu, mazito na ya hatari mno kama hayo, Imam huyo mtukufu hakuruhusu kuakhirishwa Sala ya Adhuhuri, bali aliisimamisha kwa ushujaa mkubwa, na funzo hilo linatekelezwa hadi leo na wapenzi wa watu wa kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW. Sambamba na kumbukumbu za Siku ya Ashura, Waislamu katika kona zote za Iran, leo Adhuhuri wamesali Sala za jamaa katika maeneo ya wazi na ya ndani kote nchini, kufuata sunna hiyo ya Imam Husain AS. 

Mapambano ya Karbla ya Imam Husain AS na wafuasi wake watiifu yalitokea mwaka 680 AD, na watukufu hao walipigana kishujaa katika vita vya kidhulma walivyolazimishwa kupigana na maelfu ya wanajeshi wa khalifa wa Bani Umayyah, Yazid mwana wa Muawiya, mwana wa Abu Sufyan ambaye alikuwa adui mkubwa wa Mtume Muhammad na Waislamu na aliendeleza vita dhidi ya Uislamu hadi dakika ya mwisho na kufikia hadi ya kuwa miongoni mwa watu ambao walisamehewa tu na Bwana Mtume baada ya ukombozi wa Makkah, ili kuonesha kuwa Uislamu ni dini ya kusameheana na kuhurumia wengine.

Tags