Rais Rouhani: Kuweko mifarakano katika eneo, ndilo takwa la Marekani na Uzayuni
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuweko mifarakano baina ya mataifa ya Mashariki ya Kati ndilo takwa la Marekani na Uzayuni.
Rais Rouhani amesema hayo leo akihutubia gwaride la majeshi ya Iran hapa Tehran, kwa mnasaba wa kuanza maadhimisho ya 39 ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu na kusisitiza kwamba, mantiki ya Iran ni usalama wa ndani kwa ajili ya Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz.
Rais Rouhani amebainisha kwamba, uwepo wa vikosi vya kigeni katika eneo hili unaweza kulisababisha eneo hili matatizo.
Kadhalika Rais wa Iran amesema bayana kwamba, nguvu ya vikosi vya ulinzi na taifa kubwa la Iran ni mambo ambayo yanamfanya adui asithubutu kulishambulia kijeshi taifa hili.

Aidha amesema, wananchi wa Iran wamedumisha umoja na mshikamano na wamesimama kidete na hivyo hawatishwi na makeke ya Wamagharibi na Wamashariki, hawaogopeshwi na silaha zao na wala si wenye kusalimu amri mbele ya dola za viongozi wa Kiarabu wenye fikra mgando.
Ameongeza kuwa, vikosi vya Marekani ndivyo vimeyumbisha usalama na amani katika nchi za Afghanistan, Syria, Iraq na Ghuba ya Uajemi. Rais Rouhani amezitaka nchi ajinabi kuondoka mara moja katika eneo hili la Asia Magharibi iwapo ni wakweli katika matamshi yao, kwamba wanataka kuona usalama na uthabiti unaimarika katika eneo, badala ya kuligeuza eneo hili kuwa soko la silaha zao.