Iran kuendelea kupunguza uwajibikaji wake kwa JCPOA
(last modified Sun, 06 Oct 2019 08:04:04 GMT )
Oct 06, 2019 08:04 UTC
  • Iran kuendelea kupunguza uwajibikaji wake kwa JCPOA

Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema kuwa, awamu ya nne ya kupunguza Iran kutekeleza ahadi zake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA itaanza kutekelezwa mwezi ujao kama ilivyopangwa na kwamba kwa sasa hakuna kituo chochote kilichobadilika.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran akisema hayo mapema leo katika mazungumzo yake na maafisa wa serikali ya Tehran, wataalamu wa sheria na balozi wa Finland hapa nchini, Keijo Norvanto wakati wa kuanza Warsha ya Sheria za Nyuklia inayofanyika katika ofisi za AEOI hapa Tehran.

Hata hivyo amesisitiza kuwa, licha ya vuta nikuvute na changamoto zilizopo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kufungamana na mapatano hayo ya kimataifa.

Kamalvandi ameutaka upande wa pili wa  makubaliano hayo kutekeleza wajibu na ahadi zao na kueleza bayana kwamba, hatua ilizochukua Iran katika kupunguza uwajibikaji wake zinaweza kuangaliwa upya iwapo pande nyingine husika za mapatano hayo zitachukua hatua za kivitendo za kunusuru JCPOA.

Iran kuchukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake mwezi ujao

Kauli ya Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran ni radiamali kwa vitisho vya nchi za Ulaya ambazo zimedai kuwa zitajiondoa kwenye makubaliano hayo ya nyuklia iwapo Iran eti haitafungamana kikamilifu na mapatano hayo.

Viongozi wa nchi za EU wamesema iwapo Iran itachukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo mwezi Novemba mwaka huu, basi nchi hizo za Ulaya zitaanza kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.

 

Tags