Iran yakaribisha mazungumzo na Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56565-iran_yakaribisha_mazungumzo_na_saudi_arabia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha juhudi za upatanishi za kuandaa mazungumzo baina ya Tehran na Saudi Arabia zikiwemo zile zinazofanywa na Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan, ambaye leo Jumamosi anatarajiwa kuwasili hapa Tehran kwa ajili ya kuonana na viongozi wa ngazi za juu wa Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2019 23:37 UTC
  • Iran yakaribisha mazungumzo na Saudi Arabia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha juhudi za upatanishi za kuandaa mazungumzo baina ya Tehran na Saudi Arabia zikiwemo zile zinazofanywa na Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan, ambaye leo Jumamosi anatarajiwa kuwasili hapa Tehran kwa ajili ya kuonana na viongozi wa ngazi za juu wa Iran.

Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya TRT World ya Uturuki na kuongeza kuwa, sisi muda wote tumekuwa tukisema kwamba hatuna tatizo lolote katika kufanya mazungumzo na Saudi Arabia. Saudia ni jirani yetu. Tutaendelea kuwa pamoja katika eneo hili milele.

Ameongeza kuwa, hatuna njia nyingine isipokuwa kufanya mazungumzo ya pamoja. Muda wote sisi tuko tayari kufanya mazungumzo na Saudia kwa njia ya moja kwa moja au kupitia wapatanishi.

Taifa kubwa la Iran linakaribisha mazungumzo na majirani zake wote

 

Itakumbukwa kuwa, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran muda wote ni kuishi kwa usalama na amani na majirani zake na muda wote imekuwa ikipigania kutatuliwa matatizo ya eneo hili kwa njia ya mazungumzo na majirani zake wote ikiwemo Saudia, lakini ni viongozi wa Saudi Arabia ndio ambao muda wote wamekuwa wakichukua misimamo ya kiuadui dhidi ya Tehran tena bila ya sababu yoyote ya maana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, kamwe hatujawahi kupinga juhudi za upatanishi… Muda wote tumekuwa wa wazi katika suala hilo, na muda wote tunasema kuwa tuko tayari kwa mazungumzo na majirani zetu Saudia, iwe kwa njia ya moja kwa moja au kupitia wapatanishi.

Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Pakistan alinukuliwa na gazeti la Dawn la nchi hiyo akisema kuwa, wakati alipotembelea Riyadh hivi karibuni, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammad bin Salman alimuomba asaidie kutatua hitilafu zilizopo baina ya Riyadh na Tehran.