Oct 18, 2019 16:41 UTC
  • Ali Shamkhani
    Ali Shamkhani

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameashiria uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa hakuna nchi inayoweza kuusababishia madhara usalama wa Iran.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea vituo vya kuhudumia mazuwari wanaoelekea karbala kuzuru Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika kituo cha mpakani cha  Chazabeh kusini magharibi mwa Iran, Shamkhani amesema kuwa, katika shughuli ya Arubaini ya mwaka huu mamilioni ya mazuwari kutoka Iran na nchi nyingine wanashiriki katika tukio hilo kubwa na hakuna tatizo lolote la kiusalama hapa nchini na huko Iraq.  

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameyataja matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (a.s) kuwa ni mhimili kwa wapigania ukombozi, watetezi wa wananchi wa Palestina na wainzani dhidi ya Uzayuni. 

Ali Shamkhani aidha amepongeza na kushukuru jitihada za serikali na wananchi wa Iraq za kufanikisha marasimu ya Arubaini ya Hussein (a.s).

Tarehe 20 Safar sawa na Oktoba 19 mwaka huu wa 2019 ni siku ya marasimu ya Arubaini ya kukumbuka tukio la kuuawa shahidi Imam Hussein (a.s) na wafuasi wake katika jangwa la Karbala. Waislamu wengi na wafuasi wa dini nyingine za Mwenyezi Mungu wamekuwa wakielekea katika Haramu tukufu la Imam huyo huko Karbala tangu siku kadhaa zilizopita kwa ajili ya kushiriki kwenye shughuli hiyo wakitembelea kwa miguu umbali wa karibu kilomita 80 kutoka mji wa Najaf hadi Karbala. 

Mazuwari kutoka nchi mbalimbali katika matembezi ya Arubaini  
 

Takwimu rasmi zilizotolewa na duru za Iraq zinaeleza kuwa, karibu mazuwari milioni 14 mwaka jana walishiriki kwenye matembezi ya Arubaini ya Hussein (a.s) ambao ni mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini duniani unaofanyika kila mwaka. 

Tags