"Nchi za Ulaya hazina muamana, zinashirikiana na Marekani kuishinikiza Iran"
(last modified Sun, 20 Oct 2019 07:46:15 GMT )
Oct 20, 2019 07:46 UTC

Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema nchi za Ulaya hazina muamana na zimeshindwa kutekeleza wajibu wao kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Hossein Amir-Abdollahian amezitaja Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kama washiriki wa Marekani katika kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu, badala ya kutekeleza ahadi zao kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Amesema nchi hizo za Ulaya zinafanya kazi bega kwa bega na Marekani katika kuidhoofisha Iran kupitia vikwazo, njama ambazo anasisitiza kuwa zitagonga mwamba.

Kadhalika amezikosoa vikali nchi hizo kwa kushindwa kutekeleza barabara mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX). Msaidizi huyo maalumu wa Spika wa Bunge la Iran amesema Tehran inahitaji kuchukua hatua madhubuti za kupambana na muundo wa ugaidi wa kiuchumi wa madola ya kibeberu uliopewa jina la vikwazo.

US ilijiondoa kwenye JCPOA Mei mwaka jana 2018

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kadhaa wamekosoa utendaji usioridhisha wa Ulaya katika miezi iliyopita na kutotekelezwa mfumo wa INSTEX; hatua iliyoipelekea Tehran kuchukua pia hatua za kivitendo mkabala wake.

Septemba 6, Tehran ilianza kutekeleza hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA, na hatua ya nne inatazamiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao wa Novemba.

Tags