Japan yataka kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya JCPOA
(last modified Thu, 24 Oct 2019 16:41:55 GMT )
Oct 24, 2019 16:41 UTC
  • Japan yataka kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya JCPOA

Waziri Mkuu wa Japan ametoa mwito kwa nchi zote husika kutekeleza kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya Iran JCPOA.

Abe Shinzo ametoa mwito huo leo Alkhamisi katika mazungumzo yake na Laya Joneidi, Makamu wa Rais wa Iran anayehusika na Masuala ya Sheria ambaye yuko Japan kushiriki sherehe ya kutawazwa rasmi mfalme mpya wa Japan, Naruhito. 

Abe Shinzo amesema serikali ya Tokyo inaheshimu na kuunga mkono makubaliano hayo ya kimataifa na inataka kuziona pande husika zinaheshimu kikamilifu mapatano hayo.

Kadhalika Waziri Mkuu wa Japan amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Tokyo katika uga wa siasa. Iran na Japan hivi sasa zinajivunia miaka 90 ya kuwa na uhusiano wa kidiplomasia.

Mei 2018, Donald Trump alichukua uamuzi wa upande moja wa kuiondoa Marekani katika JCPOA

Kwa upande wake, Laya Joneidi, Makamu wa Rais wa Iran anayehusika na masuala ya sheria amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaheshimu na inaendelea kufungamana na JCPOA, jambo ambalo limethibitishwa mara kadhaa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Aidha ametoa mwito wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili wa Iran na Japan katika nyuga mbalimbali.

Tags