Araqchi: Iran imepunguza uwajibikaji wake ili kuyalinda makubaliano ya JCPOA
(last modified Tue, 12 Nov 2019 12:04:11 GMT )
Nov 12, 2019 12:04 UTC
  • Araqchi:  Iran imepunguza uwajibikaji wake ili kuyalinda makubaliano ya JCPOA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala ya Kisiasa amesema kuwa lengo la Tehran kupunguza ahadi na uwajibikaji wake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kwa ajili ya kuyalinda makubaliano hayo.

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya RT ya Russia  hii leo, Sayyid Abbas Araqchi amesema kuwa kwa mujibu wa kipengee cha 36 cha makubaliano ya JCPOA Iran ina haki ya kupunguza kikamilifu au kwa kiwango fulani uwajibikaji wake ndani ya JCPOA iwapo pande nyingine husika katika makubaliano hayo zitashindwa kutekeleza majukumu yao. Kwa msingi huo,  Iran imetekeleza suala hilo hatua kwa hatua ili kubakie fursa ya diplomasia kuchukua mkondo wake. 

Araqchi amebainisha kuwa hakuna shaka yoyote kwamba Iran haina lengo la kumiliki silaha za nyuklia; bali inapinga silaha hizo. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa ameongeza kuwa siasa za nyuklia za nchi hii ziko wazi; na kwa mujibu wa fatwa ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni haramu kutumia silaha za nyuklia na miradi hiyo pia haina nafasi katika aidiolojia ya usalama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei 
 

Sayyid Abbas Araqchi amesema kuwa Iran imetekeleza ahadi na majukumu yake yote kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia hata hivyo kwa bahati mbaya pande husika ndani ya JCPOA hazitatekeleza ahadi zao. Aidha katika ripoti zake ambazo tangu awali imekuwa ikizitoa kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA siku zote imekuwa ikitangaza wazi kwamba Iran imefungamana na kutekeleza kikamilifu majukumu yake; kwa msingi huo hakuna yoyote anayeweza kutilia shaka jambo hilo.  

Tags