Iran yajibu matamshi ya kichochezi ya Pompeo
-
Sayyid Abbas Mousavi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekemea msimamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo wa kuliunga mkono kundi dogo la watu waliohusika na machafuko katika miji kadhaa hapa nchini na kusema: Hatua za baadhi ya watu waharibifu na wanaozusha fujo wanaoungwa mkono na mithili ya Mike Pompeo hazioani na mwenendo wa wananchi wengi wa Iran wenye utambuzi na muono wa mbali.
Sayyid Abbas Mousavi amelaani uungaji mkono na matamshi ya Pompeo ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kusema wananchi wa Iran wanajua vyema kwamba, matamshi yaliyojaa ria na hadaa ya afisa huyo wa Marekani hayaakisi mshikamano wa kweli na wananchi wa Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria nia mbaya ya serikali ya Marekani hususan Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala huo dhidi ya wananchi wa Iran na kusema: Afisa huyo ameeleza mshikamano wake na wananchi wa Iran ambao wako chini ya mashinikizo ya ugaidi wa kiuchumi wa Marekani ilihali hapo kabla Pompeo mwenyewe alikuwa ametamka waziwazi kwamba Wairani wanapaswa kuteswa kwa njaa ili wasalimu amri mbele ya Marekani.
Jumamosi Mosi iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo aliendeleza sera za Washington za kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine kwa kutuma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa Twitter akiashiria maandamano ya hapa na pale katika baadhi ya miji ya Iran kutokana na marekebisho ya bei ya mafuta na kudai kuwa Washington inawaunga mkono wa nawanchi wa Iran!