Ayatullah Khatami: Njama za maadui za kutikisa Mfumo zimegonga mwamba
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57422-ayatullah_khatami_njama_za_maadui_za_kutikisa_mfumo_zimegonga_mwamba
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran ameashiria njama za maadui za kutaka kutoa pigo kwa Mfumo wa Uongozi hapa nchini na kusema: "Hakuna mtu anayepinga watu kushiriki maandamano ya amani, lakini ni wazi maadui walitaka kushinikiza wimbi la ghasia na kuibua ukosefu wa usalama hapa nchini Iran."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 22, 2019 09:57 UTC
  • Ayatullah Khatami: Njama za maadui za kutikisa Mfumo zimegonga mwamba

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran ameashiria njama za maadui za kutaka kutoa pigo kwa Mfumo wa Uongozi hapa nchini na kusema: "Hakuna mtu anayepinga watu kushiriki maandamano ya amani, lakini ni wazi maadui walitaka kushinikiza wimbi la ghasia na kuibua ukosefu wa usalama hapa nchini Iran."

Ayatullah Ahmad Khatami amesema kwa mujibu wa Sura ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu, wananchi wa Iran wamedhaminiwa uhuru na haki ya kufanya maandamano kwa amani, madhali hawatabeba silaha wala kuibua ghasia au kuvunja sheria za Kiislamu wakati wa maandamano hayo.

Amesema katika hali ambayo katiba ya Iran inaruhusu maandamano ya amani, lakini vyombo vya usalama hulazimika kuingilia kati na kuwashughulikia wafanya fujo na watu wanaoibua ghasia kwenye maandamano kama hayo.

Ayatullah Khatami amesema, "Dunia inajua kuwa Jamhuri ya Kiislamu ina Mfumo madhubuti ambao hauwezi kutikiswa au kuyumbishwa na upuuzi wa maadui. Wakijaribu tena (maadui) wafahamu kuwa watafeli tena."

Maandamano ya kuiunga mkono serikali ya Iran

Ijumaa iliyopita, serikali ya Iran iliamua kukata ruzuku ya mafuta iliyokuwa ikiitoa kwa wananchi. Baadhi ya wananchi waliandamana kwa amani kulalamika kuhusu kuondolewa ruzuku hiyo iliyopelekea kuongezeka kwa bei ya mafuta, lakini wahuni na vibaraka wa maajinabi walitumia vibaya malalamiko hayo ya wananchi na kuibua ghasia ambazo zimelaaniwa kote nchini.

Hii ni katika hali ambayo, maandamano mengine ya amani yamefanyika katika miji mbalimbali ya nchi, kwa ajili ya kuunga mkono Mfumo wa Kiislamu na kuwakosoa wafanya fujo wanaochochewa na Marekani na nchi nyinginr za Magharibi.