Apr 26, 2016 07:53 UTC
  • Baada ya US, Russia pia kununua maji mazito kutoka Iran

Russia imetangaza kuwa inapania kununua maji mazito ya nyuklia ya Iran, siku chache baada ya Marekani kufanya muamala na Jamhuri ya Kiislamu juu ya bidhaa hiyo.

Kanali ya televisheni ya Press TV ya Iran imenukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia inayosema kuwa, serikali ya Moscow inapanga kununua tani 40 za maji mazito ya Iran. Wakati huo huo, Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kwa sasa Tehran na Moscow zinajadiliana kuhusu suala hilo la Russia kununua maji mazito ya Iran.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Washington hivi karibuni ilitangaza azma yake ya kununua maji mazito ya nyuklia ya Iran kwa dola milioni 8.6 za Marekani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa inatarajia kuwa tani 32 za maji mazito kutoka Iran zitakabidhiwa kwa nchi hiyo wiki ijayo. Elizabeth Trodo amesema kuwa maji hayo mazito yatakidhi haja ya ndani ya Marekani kwa ajili ya viwanda na utafiti na kuongeza kwamba muamala huo ni matunda muhimu.

Habari ya Iran kuiuzia Marekani makumi ya tani za maji mazito ya nyuklia pia imethibitishwa na maafisa husika hapa nchini kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.

Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, baada ya Russia na Marekani, yumkini madola mengine makubwa yakaagiza maji mazito ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu.

Tags