IRGC: Iran ya Kiislamu imefikia kilele cha nguvu na uwezo mkubwa
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) sambamba na kuashiria vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya raia wa nchi hii amesema kuwa, hii leo Iran ya Kiislamu iko kwenye kilele cha nguvu na uwezo mkubwa.
Meja Jenerali Hossein Salami ameyasema hayo katika kongamano la wenye medali ya dhahabu ya usalama na utendajikazi mjini Ahwaz, kusini magharibi mwa Iran na kuongeza kwamba, kwa kutumia muono wa kitaifa na kwa kutegemea muongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchi hii imeweza kubadilisha vitisho kuwa fursa.
Kadhalika ameashiria matukio ya hivi karibuni ndani ya Iraq na kubainisha kwamba, maadui wa Iraq wanafeli kisha kuihusisha Iran na kushindwa kwao. Hata hivyo amesisitiza kwa kusema: "Iran inatangaza kwamba haiingilii masuala ya ndani ya nchi yoyote ile." Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameongeza kuwa, kwa mujibu wa maelekezo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran haitaanzisha vita kwa vyovyote vile, lakini imejiweka tayari kwa ajili ya kujitetea.