Mwamko wa walimwengu na kuchanganyikiwa NATO na Marekani kuhusu Luteni Soleimani
Radiamali na hisia zilizooneshwa na baadh iya viongozi wa nchi za Magharibi baada ya Marekani kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kwa mara nyingine zimeonesha undumilakuwili wa viongozi wa nchi za Magharibi kuhusu madai yao ya kupambana na magaidi.
Shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa kamanda shujaa aliyepambana vilivyo na ugaidi kwa sura mbalimbali, hususan ugaidi wa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) lililoundwa na Marekani. Magaidi hao walimiminika katika eneo la Asia Magharibi kutoka miji na maeneo tofauti ya Ulaya kuja kufanya jinai na kuendesha vita dhidi ya wananchi wa Iraq na Syria kwa niaba ya nchi hizo za Magharibi. Kushindwa kwa sura mbalimbali ugaidi katika eneo la Asia Magharibi kumezuia mipaka ya ukosefu wa amani kufika ndani ya nchi za Ulaya. Kwa kweli kilichotarajiwa na watu wenye insafu, nia nzuri na moyo safi ni kuziona nchi za Magharibi zikimshukuru kila aliyefanya juhudi za kupambana na magaidi katika eneo hili hasa huko Iraq na Syria. Lakini cha kushangaza ni kuona kuwa, nchi hizo za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinaonesha chuki na uadui mkubwa kwa watu kama Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyetoa mchango wa kipekee wa kusambaratishwa magaidi wa ISIS katika eneo hili.
Ukweli ni kwamba utulivu na amani iliyoko katika nchi za Ulaya hivi sasa ni matunda ya juhudi wa wanamapambano wa Kiislamu akiwemo Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ambao wameendesha mapambano kwa nia safi na kuwasambaratisha magaidi wa Daesh na hivyo hawakuruhusu ugaidi na jinai za wakufurushaji hao kufika ndani ya nchi za Ulaya.
Kumalizwa shari ya ugaidi wa magenge ya Daesh na Jabhat al Nusr ambayo kuna wakati yalikuwa yanadai kwamba eneo lao linajumuisha zaidi ya nchi 80 duniani hususan nchi za Ulaya, ndiko kulikoleta usalama katika miji mikuu ya nchi za Magharibi hasa kwa kuzingatia kwamba magaidi hao walikuwa na mipango maalumu ya kufanya mashambulizi chungu nzima ya kigaidi barani Ulaya.
Hata hivyo, moja ya uthibitisho wa siasa za nyuso mbili za nchi za Magharibi, ni hatua ya Katibu wa Shirika la Kijeshi la NATO ya kujaribu kuhalalisha kuuliwa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, ikiwa ni uungaji mkono wa wazi wa shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi kwa jinai hiyo ya Marekani. Luteni Jenerali Soleimani ameshambuliwa na Marekani na kuuliwa shahidi kidhulma akiwa katika eneo la kiraia, akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq na akiwa ameandamana na viongozi rasmi wa nchi hiyo. Lakini NATO kama Marekani zimedharau sheria zote za kimataifa katika suala hilo. Hata hivyo kitendo hicho cha NATO cha kuunga mkono kuuliwa kigaidi mgeni rasmi wa serikali ya Iraq tena uraiani si katika medani ya vita, si kitu cha kushangaza, kwani ni hiyo hiyo NATO kwa uongozi wa Marekani ndiyo inayoendelea kufanya uharibifu mkubwa katika maeneo mbalimbali duniani hususan nchini Afghanistan kwa miaka mingi sasa.
Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Jumatano usiku, sambamba na kulaani kitendo cha Katibu wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO, Jens Stoltenberg, cha kuunga mkono jinai ya Marekani ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani alisema: Katika kipindi cha miaka mingi sasa, NATO haijawahi kuwa na matunda yoyote mazuri isipokuwa kufanya uharibifu, vita, uangamizaji wa miundombinu na kuwasababishia watu wa eneo hili, ukosefu mkubwa wa amani.
Amma kilicho muhimu zaidi hapa ni hisia na mwamko wa walio wengi duniani. Walimwengu hivi sasa wameamka na wameonesha wazi kukasirishwa na jinai ya Marekani ya kumuua kidhulma mtu kama Luteni Jenerali Qassem Soleimani ambaye alikuwa kamanda shupavu anayepigana kikweli kweli na ugaidi duniani. Na inaonekana wazi kwamba undumilakuwili wa Marekani, NATO na wenzao unazidi kufichuka huku madola ya kibeberu yakizidi kuchanganyikiwa kwa kuona kuwa hayawezi tena kuficha siasa zao za nyuso mbili wala misimamo yao ya kindumilakuwili mbele ya walimwengu.