Venezuela yaionya Marekani na kuitaka iache kuingilia masuala yake ya ndani
(last modified Sat, 11 Jan 2020 12:33:11 GMT )
Jan 11, 2020 12:33 UTC
  • Venezuela yaionya Marekani na kuitaka iache kuingilia masuala yake ya ndani

Serikali ya Venezuela imeionya Marekani na kuitaka iache mchezo wake wa kuingilia masuala ya ndani ya Caracas.

Onyo hilo limetolewa na Jorge Arreaza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela ambaye ameitaka Marekiani ijiepushe na njama zozote zile za kutaka kuingilia uchaguzi wa Bunge wa nchi hiyo.

Jorge Arreaza ameeleza kuwa, hatua ya serikali ya Marekani ya kuzitumia ujumbe baadhi ya nchi ikieleza takwa lake la kufanyika uchaguzi huru nchini Venezuela inalenga kuingilia uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanyika mwaka huu.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela amebainisha kwamba, Marekani haijaacha mkakati wake wa hapo kabla wa kuingilia uchaguzi wa Venezuela na masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Amesema, serikali ya Marekani inafuatilia suala la kuweko serikali ya mpito nchini Venezuela ili kupitia njia hiyo ihakikishe kwamba, kunafanyika uchaguzi kama inavyotaka yenyewe.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela amesisitiza kuwa, serikali ya Caracas haitaruhusu hilo litokee, kwani Venezuela siyo kibaraka wa Marekani.

Tarehe 23 Januari mwaka jana, Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani nchini humo alijitangaza kuwa rais wa Venezuela akipata uungaji mkono wa wazi wa serikali ya Marekani na waitifaki wake, hatua ambayo ilitajwa na serikali na taifa hilo kuwa ni mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Nicolás Maduro.

Tags