Rouhani: Iran ina irada ya kustawisha ushirikiano wa pande zote na Syria
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran na irada ya kuimarisha na kustawisha uhusiano wa pande zote na Syria.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Emad Khamis, Waziri Mkuu wa Syria na kuongeza kuwa: "Leo uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi zingine na kutaka kuchukua udhibiti wa visima vya mafuta Syria ni jambo ambalo liko wazi." Amesema Marekani katu haijali maslahi ya mataifa ya eneo.
Rais Rouhani ameongeza kuwa kama ambavyo Iran imesimama bega kwa bega na Syria katika vita dhidi ya ugaidi, pia itaendelea kusimama pamoja na mataifa yanayodhulumiwa ambayo yanapamabana na madola ya kibeberu na kiistikbari.
Katika mkutano huo, Emad Khamis, Waziri Mkuu wa Syria amewasilisha salamu za rambi rambi za Syria kufuatia kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: "Kuuawa shahidi Luteni Jenerali Soleimani ni maafa na msiba mkubwa kwa mataifa yote ambayo yanataka uhuru kamili duniani."
Emad Khamis amesema hatua ya Iran kushambulia kwa makombora kituo cha Jeshi la Marekani nchini Iraq, ikiwa ni katika kulipiza kisasi mauaji ya Shahidi Soleimani, ni ujumbe wa wazi kwa serikali na mataifa ya eneo na dunia. Ameongeza kuwa, hatua hiyo ya Iran pia ina ujumbe wa wazi kwa uistikbari wa kimataifa kuwa hauna nafasi yoyote katika eneo la Asia Magharibi.
Waziri Mkuu wa Syria amesema mapambano dhidi ya magaidi yataendelea Asia Magharibi na kuongeza kuwa majeshi ya Marekani yanaikalia Syria kwa mabavu na kwa msingi huo mataifa yote yanapaswa kukabiliana na uwepo huo haramu wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.