Iran: Kujitoa Marekani hakutushughulishi, kama Ulaya wataheshimu JCPOA nasi tutaheshimu
Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, nchi zinazounda kundi la 4+1 katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA zinapaswa kuheshimu vilivyo makubaliano hayo na kama nchi za Ulaya zitaheshimu vipengee vya mapatano hayo, Tehran nayo bila ya shaka yoyote itaheshimu.
Mahmoud Vaezi alisema hayo jana pembeni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri na kuwaambia waandishi wa habari kwamba, Iran itatekeleza ahadi zake katika JCPOA iwapo tu kundi la 4+1 nalo litaheshimu.
Amma kuhusiana na mpango wa kulirejesha faili la JCPOA kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Vaezi amesema, iwapo Marekani na nchi zilizobakia kwenye mapatano hayo zitalirejesha suala la miradi ya nyuklia ya Iran kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, basi zijue kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitokaa kimya na itatoa majibu makali kwa hatua yao hiyo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisubiri mwaka mzima kuona ni hatua gani zitachukuliwa na kundi la 4+1 baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuirejesha Tehran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo. Hata hivyo kundi hilo hasa nchi za Ulaya hazikuchukua hatua yoyote ya maana ya kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja na vya kidhulma vya Marekani dhidi ya Iran. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Tehran nayo imeamua kupunguza ahadi zake kwenye JCPOA kujibu hatua hizo za nchi za Ulaya na Marekani.
Amma kuhusu uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi mbili za Kiislamu za Iran na Oman, Mkuu huyo wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Tehran na Muscat zinapaswa kuongeza ushirikiano wao katika kulinda usalama wa Lango Bahari la Hormuz.