Russia: Hakuna haja ya kufanya makubaliano mapya na Iran
Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Wakala wa Kimataifa wa Niashati ya Atomiki (IAEA) amesema kuwa Moscow inaamini kwamba hakuna haja ya kufanyika makubaliano mapya ya nyuklia na Iran, na badala yake mapatano ya JCPOA ni lazima yatekelezwe.
Mikhail Ulyanov ameyasema hayo kupitia ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo sambamba na kusisitiza kuwa hakuna haja ya mapatano mapya ya nyuklia, amebainisha kwamba, mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni lazima yetekelezwe kwa kuwa makubaliano hayo ndio yanaweka wazi kikamilifu uhalisia wa amani wa miradi hiyo ya Iran. Amesema kuwa baada ya hapo, protokoli ziada ikiambatanishwa na uchunguzi mkali, itatoa dhamana inayohitajika kuhusu malengo ya amani ya miradi hiyo ya nyuklia ya Iran. Kadhalika mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Wakala wa Kimataifa wa Niashati ya Atomiki (IAEA) ameongeza kuwa wanachama wa mapatano ya nyuklia wanatakiwa kufahamu kwamba baada ya kutekelezwa mapatano hayo ya JCPOA, miradi yote ya nyuklia ya Tehran itakuwa sawa na miradi ya nchi nyingine zisizomiliki nishati hiyo wanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia NPT.
Itakumbukwa kuwa Marekani ilijiondoa kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hapo tarehe 8 Mei 2018 na kisha kurejesha vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Nchi za Ulaya licha ya kupinga siasa hizo mbovu za Rais Donald Trump wa Marekani, lakini zimeshindwa kuchukua hatua athirifu na za kutosha kwa ajili ya kutekeleza ahadi zao ili kuidhaminia Iran maslahi yake katika kukabiliana na vikwazo hivyo vya Marekani.