Velayati: Mapinduzi ya Kiislamu yamepiga hatua kubwa ndani ya miaka 40
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, taifa hili limepata mafanikio mengi katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya miongo minne ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Dakta Ali Akbar Velayati amesema hayo leo Jumatatu hapa Tehran na kubainisha kuwa, "miaka 40 imepita tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hii leo, sote tunashuhudia matunda na mafanikio makubwa ya ushindi huo sio hapa nchini Iran tu, bali kieneo na kimataifa pia."
Amesema taifa hili limepiga hatua kubwa katika uga wa sayansi na teknolojia na hii leo, sekta ya sanyansi ya Iran inastawi mara 11 zaidi ya nchi nyingine yoyote ile duniani.
Amefafanua kuwa, ni kutokana na hayo ndiposa Iran inajivunia kuwa miongoni mwa nchi chache zenye teknolojia ya nishati ya nyuklia, teknolojia ya nano, ufanisi mkubwa katika uga wa anga za mbali pamoja na ustawi katika sekta ya tiba na madawa.
Ali Akbar Velayati ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kiistratijia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamewapa Waislamu na wapigania haki kote duniani matumaini.
Maandamano makubwa ya 22 Bahman katika kuadhimisha miaka 41 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yamepangwa kufanyika kesho katika miji na vijiji 5,200 kote Iran.