Palestina yaishukuru Iran kutokana na misimamo yake chanya katika kutetea taifa hilo
Balozi wa Palestina mjini tehran amepongeza misimamo imara na tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu haki za taifa hilo hususan msimamo wake wa kupinga mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne.
Salah al-Zawawi ameyasema hayo katika marasimu ya mkutano wa kutoa pongezi kwa Rais Hassan Rouhani wa Iran uliowahusisha mabalozi wa kigeni na viongozi wa taasisi za kimataifa mjini Tehran kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 41 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Al-Zawawi ameongeza kuwa hii leo ulimwengu umegubikwa na vita, mapigano na ukiukaji wa haki za mataifa kutoka kisasi hadi kizazi, bila ya kuwepo kwa njia za utatuzi wake.
Balozi wa Palestina mjini Tehran sambamba na kutangaza kutupilia mbali mpango wa Muamala wa Karne kutokana na kupinga mapambano ya kihistoria ya wananchi wa Palestina amebainisha kuwa, mpango huo unahimiza kukiukwa maazimio ya Umoja wa Mataifa likiwemo suala la kutupiliwa mbali haki ya kurejea wakimbizi wa Palestina kwenye ardhi zao za jadi. Itakumbukwa kuwa tarehe 28 Januari Rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni walizindua mpango huo wa kibaguzi wa Muamala wa Karne ambao umeendelea kupingwa duniani kote.