"Muamala wa Karne umewaunganisha Waislamu kote duniani"
Mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS mjini Tehran amesema mpango wa kibaguzi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina uliopewa jina la Muamala wa Karne umekuwa chachu na sababu ya kuungana Waislamu kote duniani bila kujali tofauti zao za kimadhehebu.
Khaled al-Qaddumi amesema hayo katika Kongamano la 'Chuo cha Muqawama' lililofanyika katika mji mtakatifu wa Qum, yapata kilomita 140 kusini mwa mji mkuu Tehran na kuongeza kuwa, "Muamala wa Karne" ni mstari unaotenganisha haki na batili.
Amesema kinyume na matarajio ya Wamarekani na Wazayuni, mpango huo ghalati uliojaa hadaa umewaunganisha Waislamu kote duniani ambao wameapa kuusambaratisha na kuhakikisha kuwa hautekelezwi.
Mwakilishi wa Harakati ya HAMAS mjini Tehran ameeleza bayana kuwa, "kwa kuzindua Muamala wa Karne, na kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) sambamba na kushadidisha mashinikizo dhidi ya watu wa eneo la Asia Magharibi, Rais Donald Trump wa Marekani alidhani atapata ushindi katika eneo, lakini malengo ya njama hizo batili yamegonga mwamba."
Ameongeza kuwa, Waislamu na wapenda haki katika medani ya kieneo na kimataifa wameupiga chini mpango huo wa Kimarekani na Kizayuni unaokusudia kuwapokonya Wapalestina haki zao zote za msingi.
Itakumbukwa kuwa tarehe 28 mwezi uliopita wa Januari, Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu walizindua mpango huo eti wa amani wa Muamala wa Karne, ambao unaendelea kulaaniwa na kukosolewa kote duniani.