Rouhani: Iran haijafunga mlango wa mazungumzo ya kuinusuru JCPOA
(last modified Sun, 23 Feb 2020 13:32:27 GMT )
Feb 23, 2020 13:32 UTC
  • Rouhani: Iran haijafunga mlango wa mazungumzo ya kuinusuru JCPOA

Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijafunga mlango wa kufanya mazungumzo na nchi za Ulaya kwa shabaha ya kuyanusuru makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais Rouhani amesema hayo katika mazungumzo yake na Stef Blok, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi hapa jijini Tehran na kuongeza kuwa, "tunaamini kuwa makubaliano ya JCPOA yana maslahi kwa eneo na dunia nzima kwa ujumla."

Dakta Rouhani amesema hatua za uhasama za Marekani dhidi ya mapatano hayo ya kimataifa hazijakuwa tu na taathira hasi kwa mataifa mengine duniani, bali pia kwa Wamarekani wenyewe.

Ameeleza bayana kuwa, "zaidi ya miezi 21 baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 8 mwaka 2018, nchi za Ulaya kwa bahati mbaya zimefeli kuchukua hatua za kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran katika mapatano hayo."    

Ameongeza kuwa, iwapo Marekani itaacha mienendo yake ya kigaidi na uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi za Asia Magharibi, basi eneo hili litakuwa pahala salama pa kuishi.

Rais Rouhani na Stef Blok, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi

Licha ya kutoa matamshi ya kupinga maamuzi ya Marekani kuhusu JCPOA, lakini nchi hizo za Ulaya hazijachukua hatua za kivitendo kutekeleza ahadi zao za kulinda mapatano hayo, jambo ambalo liliilazimisha Iran kupunguza uwajibikaji wake hatua kwa hatua kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Stef Blok amegusia masuala ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Uholanzi na Iran na kusisitiza kuwa, anatumai serikali yake itakuwa na nafasi muhimu ya kufanikisha mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX).

Tags