Meja Jenerali Salami: Iran hivi sasa ipo katika vita vya kibiolojia
-
Meja Jenerali Hossein Salami
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema taifa la Iran lipo katika vita vya kibiolojia hivi sasa, lakini bila shaka wananchi Waislamu wa Iran wataibuka washindi.
Meja Jenerali Hossein Salami alisema hayo jana Alkhamisi mjini Kerman, kusini mashariki mwa nchi na kueleza bayana kuwa, "hii leo Iran ipo katika vita vya kibiolojia, lakini taifa hili limesimama kidete katika mapambano."
Amesisitiza kuwa, ni muhali kwa Jamhuri ya Kiislamu kushindwa katika vita vyovyote kwa kuwa inategemea nguvu na uwezo wa wananchi na pia taifa hili limejifunza kuwa gurudumu la Mapinduzi linapaswa kusonga mbele kwa kasi ya mabadiliko ya dunia.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ameongeza kuwa, maadui wanafanya kila wawezalo kulitwisha matatizo ya aina kwa aina taifa la Iran lakini amesisitiza kuwa katu taifa hili halitapigishwa magoti na mashinikizo ya maadui.
Amefafanua kuwa, "adui angali anashupalia kuliwekea taifa hili mashinikizo ya kiuchumi na kisaikolojia, na kutumia fursa yoyote inayojitokeza kushadidisha vikwazo dhidi ya Wairani. Adui anataka kubadilisha mwendo wa siasa za eneo hili kwa maslahi yake mwenyewe."
Meja Jenerali Salami ameeleza bayana kwamba, wananchi wa Iran wana utambuzi na welewa kamili kwamba, anachokifuatilia adui hapa nchini ni kuwafanya wananchi wa taifa hili wasalimu amri mbele ya matakwa yake, njama ambazo zitagonga mwamba.