Jitihada za Imarati za kudhibiti maliasili za mafuta ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59737-jitihada_za_imarati_za_kudhibiti_maliasili_za_mafuta_ya_yemen
Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unafanya kila uwezalo kudhibiti utajiri wa Yemen vikiwemo visima vya mafuta vya nchi hiyo.
(last modified 2026-01-01T11:20:11+00:00 )
Mar 14, 2020 12:07 UTC
  • Jitihada za Imarati za kudhibiti maliasili za mafuta ya Yemen

Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unafanya kila uwezalo kudhibiti utajiri wa Yemen vikiwemo visima vya mafuta vya nchi hiyo.

Vita vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia vilianza huko Yemen Machi 26 mwaka 2015. Zimesalia chini ya wiki mbili hadi kumalizika mwaka wa tano na vita hivyo kuingia mwaka wake wa sita tangu muungano huo vamizi uanzishe vita dhidi ya Yemen. Hata kama muungano huo awali uliasisiwa na nchi 9 wanachama lakini Saudi Arabia na Imarati ni nchi pekee wanachama ambazo zingali hai kwenye muungano huo, khususan kuanzia mwaka wa tatu wa kujiri vita hivyo hadi sasa. 

Saudi Arabia huko nyuma iliwahi kudai kuwa vita hivyo vilianzishwa lengo likiwa ni kurejesha utawala wa sheria au kwa ibara nyingine kumrejesha madarakani Abdu Rabbuh Mansour Hadi. Pamoja na hayo na baada ya kupita muda imebainika wazi kwamba nchi hiyo na mshirika wake Imarati zimeyaweka katika ajenda zao za kazi malengo mengine muhimu yasiyo ya kisiasa. Kitengo cha utafiti cha Al Jazeera ya Qatar kiliwahi kuripoti kuwa moja ya malengo makuu ya kistratejia yanayofuatiliwa na  Imarati huko Yemen ni kuimarisha ushawishi wa jiopolitiki katika maeneo yaliyo nje ya Bahari ya Kiarabu likiwemo eneo la Ghuba ya Aden na katika maeneo ya magharibi mwa Bahari ya Hindi. Maliasili za mafuta za Yemen ni moja ya sekta ambazo Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unafanya kila unaloweza ili kuzidhibiti. 

Abdu Rabbuh Mansour Hadi, Rais wa Yemen aliyejizulu 

Taarifa rasmi za Yemen zinaeleza kuwa nchi hiyo ina akiba iliyothibitishwa ya mafuta inayokaribia mapipa bilioni 12. Ripoti rasmi zinasema kuwa Yemen ina visima vya mafuta karibu 105; ambapo 81 kati yavyo viko katika maeneo yaliyo wazi na vingi baharini. Wakati huo huo takwimu rasmi zinaonyesha kuwa vituo 35 vya mafuta vinafanya kazi katika mikoa ya Shabwah na Hadhramaut hali iliyoishawishi Imarati kuimarisha uwepo wake katika mikoa hii miwili. Baada ya kuundwa baraza la mpito la kusini mwa Yemen sasa Imarati inafanya kila iwezalo kupitia baraza hilo kulikabidhi udhibiti wa mikoa yenye utajiri wa mafuta. 

Shoaib Salem mchambuzi wa masuala ya mafuta na nishati anasema kuwa Imarati imechukua hatua kadha wa kadha ili kufanikisha miradi yake makhsusi kupitia baraza hilo linalotajwa kuwa baraza la mpito la kusini mwa Yemen ambalo limeikalia kwa mabavu mikoa ya kusini na katikati yenye utajiri wa mafuta kwa kusaidiwa na mamluki wa kijeshi wa Kisudani. Wakati huo huo Imarati inafanya juhudi za kuvidhibiti vivuko vya kistratejia vya Yemen. Nukta muhimu ni hii kuwa katika hali ambayo Imarati inafanya jitihada za kumiliki maliasili za mafuta na vile vile  za dhahabu za Yemen; nchi hiyo maskini ya Kiarabu inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu kuwahi kushuhudiwa duniani katika miongo kadhaa ya karibuni kutokana na vita dhidi ya nchi hiyo vililivyoanzishwa na muungano vamizi chini ya uongozi wa Saudi Arabia. 

Mamluki wa Kisudan katika uvamizi wao huko Yemen 

Umoja wa Mataifa umeashiria kusambaratika uchumi wa Yemen na kusisitiza kuwa nchi hiyo kuanzia mwaka 2015 imepata hasara ya karibu dola bilioni 89. Asilimia 70 ya bajeti ya Yemen na asilimia 63 ya mapato yake zinatokana na maliasili za mafuta. Hatua na harakati zote hizi za Imarati zinaonyesha kuwa  hata kama kumrejesha madarakani Mansour Hadi lilitajwa kuwa lengo la kunzishwa vita huko Yemen na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, lakini mkabala na kadhia hiyo malengo kama ya kupora maliasili za kiuchumi za Yemen pia ni moja ya malengo makuu ya vita hivyo dhidi ya nchi hiyo.