Iran: Marekani haina hoja ya kisheria ya kuwa mshirika wa JCPOA
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani haina hoja ya kisheria ya kutaka kuwa mshirika wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter mapema leo Alkhamisi, Majid Takht-Ravanchi amemhutubu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo kwa kumuambia: Waziri Pompeo anadai kuwa, kwa misingi ya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani ni 'mshirika' katika hali ambayo azimio hilo linaashiria 'washirika wa JCPOA.'
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema Pompeo kwa makusudi amepuuza neno JCPOA, licha ya kuwa mnamo Mei 8 mwaka 2018 bosi wake (Rais Donald Trump) alitagaza wazi kuwa Marekani sio mshirika tena wa JCPOA.
Amesisitiza kuwa, kwa msingi huo Marekani iliacha kuwa mshirika wa mapatano hayo ya kimataifa na kwamba jitihada za Washington za kutaka kuishinikiza Iran kwa kutumia azimio nambari 2231 zitagonga mwamba.
Hivi karibuni pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema kuwa, uamuzi wa Marekani wa kutaka kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni matokeo ya kufeli na kushindwa vibaya siasa za "mashinikizo ya kiwango cha juu" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Muhammad Javad Zarif alisema katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Miaka miwili iliyopita, Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na Rais wake walitoa tangazo la kusitishwa ushiriki wa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA wakidhani kwamba, mashinikizo yao ya kiwango cha juu yataipigisha magoti Iran.