Bunge la Iran lapasisha muswada wa kukabili njama za Israel
Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) imepasisha kwa kauli moja muswada wa dharura wa kukabili njama za utawala wa Kizayuni wa Israel, dhidi ya amani na usalama wa kieneo na kimataifa.
Muswada huo umepasishwa kwa kura 43 za 'Ndio' na 0 ya 'Hapana' katika kikao kilichofanyika mapema leo Jumanne cha Bunge hilo.
Anga ya bunge hilo ilihinikiza kwa nara za "Mauti kwa Israel" zilizokuwa zikitolewa na wabunge wa Jamhuri ya Kiislamu wakati wa kikao hicho.
Mojtaba Zolnouri, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge hilo amesema muswada huo uliopasishwa una vipengee 14 vilivyoainisha hatua za kuchukuliwa na nchi hii, dhidi ya mienendo ya kuvuruga amani ya utawala haramu wa Israel.
Amesema utawala huo bandia unalitumia vibaya janga la corona, kuhujumu maslahi ya kitaifa na kimataifa ya Iran ya Kiislamu. Hata hivyo amesisitiza kuwa njama hizo za utawala haramu za Israel zitagonga mwamba.
Baada ya kupasishwa muswada huo, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Ali Larijani ameitaka kamati husika kuutathmini haraka iwezekanavyo, ili uwekwe kwenye ajenda ya wiki ijayo ya bunge hilo.