Rais Rouhani: Utawala mbaya zaidi na muovu zaidi Marekani ndio ulioko madarakani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60959-rais_rouhani_utawala_mbaya_zaidi_na_muovu_zaidi_marekani_ndio_ulioko_madarakani
Rais Hassan Rouhani amesema, utawala mbaya zaidi na muovu zaidi Marekani ndio ulioko madarakani na akaongeza kuwa, serikali ya Marekani siku zote ni ya kigaidi lakini kiwango hiki hakijawahi kushuhudiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2020 09:11 UTC
  • Rais Rouhani: Utawala mbaya zaidi na muovu zaidi Marekani ndio ulioko madarakani

Rais Hassan Rouhani amesema, utawala mbaya zaidi na muovu zaidi Marekani ndio ulioko madarakani na akaongeza kuwa, serikali ya Marekani siku zote ni ya kigaidi lakini kiwango hiki hakijawahi kushuhudiwa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri sambamba na kuashiria hatua na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa na Marekani katika miaka ya karibuni. Amesema: Marekani imekuwa siku zote  ikichukua hatua dhidi ya mataifa yanayojitawala na yanayodhulumiwa, lakini katika mazingira ya mripuko wa virusi vya corona pia ulioikumba dunia nzima, Marekani inaweka vizuizi mbalimbali kwa ununuzi wa dawa.

Rais Rouhani amesema, katika miaka miwili iliyopita Iran imekabiliana na utawala mbaya zaidi Marekani na akabainisha kwamba, katika historia, Marekani haijawahi kuwa katili, dhaifu na isiyo na utu kiasi hiki na hata waziri wa mambo ya nje wa utawala huo hajui hata alfabeti za siasa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia misaada ya wananchi na moyo wa kujitolea wa kada za utabibu nchini na akaeleza kwamba: Misaada yote ya mahitaji ya kimaisha, utoaji mali wa wananchi na huduma za madaktari na wauguzi wa Kiirani chimbuko lake ni utamaduni wa dini ya Kiislamu.

Dakta Rouhani ameeleza pia kwamba, moyo wa kujitolea na jitihada zinazofanywa na madaktari, wauguzi na kada ya utabibu ya Iran hazina kifani na akabainisha kwamba: Asili ya utamaduni huu ni Qur'ani Tukufu na maisha na sira ya Bwana Mtume (SAW), Amirul Muuminin (AS) na Ahlul Bayt Maasumu na Watoharifu (AS).

Kwa mujibu wa takwimu mpya za Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran hadi kufikia leo watu wapatao 110,000 wamethibitika kuambukizwa virusi vya corona, ambapo 88,357 miongoni mwao wamepata afueni na kuruhusiwa kutoka hospitali. Waliofariki dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 hapa nchini hadi sasa ni 6,733.../