Kamanda wa IRGC: Uwepo wa majeshi ya Marekani Asia Magharibi unaelekea ukingoni
Kamanda wa ngazi za juu katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameikosoa Marekani kwa kufanya mazoezi ya kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa, zama za uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo zinakaribia kumalizika.
Naibu Kamanda wa IRGC anayesimamia masuala ya kisiasa, Brigedia Jenerali Yadollah Javani ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la Tasnim na kuongeza kuwa, kile kinachofanywa na Marekani kwa kisingizio cha "mazoezi ya kijeshi ya kuimarisha usalama wa Ghuba ya Uajemi na kuwasaidia waitifaki wake, ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uwepo wake katika eneo".
Javani amesema, Wamarekani sasa wanakabiliana na hali ambayo uwepo wao katika eneo ni kwa hasara yao kwa sababu mataifa ya eneo yamechukizwa na sera za Washington.
Naibu Kamanda wa IRGC anayesimamia masuala ya kisiasa ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi yenye nguvu kieneo na sasa inalekea kuwa moja kati ya madola yenye nguvu na uwezo mkubwa katika uga wa kimataifa. Amebaini kuwa leo Marekani si dola lenye nguvu tena kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwani haiwezi kufikia malengo yote inayotaka lakini Iran inaweza kufikia malengo yake kwa mjibu wa sheria za kimataifa, kieneo na hata nje ya eneo.
Javani amesema sababu kuu ya ukosefu wa usalama na amani katika eneo ni uwepo wa madola ajinabi hasa Marekani.