May 27, 2020 08:02 UTC
  • Bunge la 11 la Iran lafunguliwa kwa hotuba ya Kiongozi Muadhamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaka Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lililoanza shughuli zake leo Jumatano kuelekeza darubini na kujikita zaidi katika masuala ya uchumi wa kimuqawama na utamaduni.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa mwito huo katika ujumbe uliosomwa Bungeni na Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatulislam Mohammadi Golpayegani katika ufunguzi wa duru ya 11 ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu leo Jumatano.

Katika ujumbe huo, Kiongozi Muadhamu amewahutubu Wabunge hao akiwaambia: Mnapaswa kuandaa mikakati ya kuboresha maisha ya watu wenye mahitaji, na hili kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya uchumi, linawezekana tu kwa kuangalia upya njia mpya za kuunua uchumi wa taifa kama kubuniwa nafasi za ajira, uzalishaji, thamani ya sarafu ya taifa, na kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa.

Kadhalika amelitaka Bunge hilo liwe na ushirikiano wa karibu na mihimili mingine ya serikali, yaani Baraza la Mawaziri na Vyombo vya Mahakama.

Kufunguliwa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameliasa Bunge hilo lisishughulishwe zaidi na mambo madogo yasio na maslahi kwa wananchi wa kawaida, sanjari na kutorohusu masuala ya kibinafsi, kichama na kimrengo kuteka ajenda za mijadala ya taasisi hiyo muhimu ya kutunga sheria.

Rais Hassan Rouhani wa Iran ameongoza maafisa wa ngazi za juu wa serikali katika kushuhudia kufunguliwa kwa Bunge hilo la 11, lenye wabunge wapya wa kuchaguliwa 268 watakaohudumu kwa muhula wa miaka minne. Kwa ujumla bunge hilo lina viti 290, ambapo mbali na wabunge wa kuchaguliwa, kuna wabunge wa kuteuliwa.

 

Tags