Iran yalaani ukatili wa polisi wa Marekani kwa kumuua raia mweusi + Video
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61246-iran_yalaani_ukatili_wa_polisi_wa_marekani_kwa_kumuua_raia_mweusi_video
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali ukatili wa polisi ya Marekani uliopelekea kupoteza maisha raia mwengine mwenye asili ya Afrika.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 27, 2020 11:36 UTC

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali ukatili wa polisi ya Marekani uliopelekea kupoteza maisha raia mwengine mwenye asili ya Afrika.

Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter leo Jumatano, wizara hiyo imesema, miaka 6 baada ya polisi ya Marekani kumkandamiza na kumuua raia mwingine mweusi wa Marekani kwa jina la Eric Garner, Mmarekani mwingine mwenye asili ya Afrika, George Floyd ameuawa kwa kutumia mbinu ile ile ya kukandamiziwa chini hadi akakata roho.

Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, inalekea kuwa ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi hauna mipaka.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema ni jambo la kusikitisha namna maafisa wa polisi wa Marekani wanavyotumia mbinu hizo za kikatili na ukandamizaji wakati wa kuwakamata washukiwa hususan Wamarekani weusi.

Ukatili wa kutisha wa polisi ya US dhidi ya Wamarekani weusi

Jumatatu iliyopita, polisi mweupe nchini Marekani alimuua kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis, jimbo la Minnesota. Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Marekani, ilimuonyesha polisi huyo akiwa amemlaza chini mtu huyo kifudifudi huku akiwa amemkandamiza vibaya shingo lake kwa goti la mguu wa kushoto.

Mtu huyo mwenye asili ya Afrika aliyejulikana kwa jina la George Floyd alikuwa akipiga kelele kwa kusema: "Umenibana shingo siwezi kupumua" "Naomba maji" na "Usiniue" hadi alipofariki dunia.