Rais Rouhani aihutubu Marekani: Biashara yetu na Venezuela haiwahusu
(last modified Thu, 28 May 2020 02:23:56 GMT )
May 28, 2020 02:23 UTC
  • Rais Rouhani aihutubu Marekani: Biashara yetu na Venezuela haiwahusu

Rais Hassan Rouhani wa Iran ameikosoa vikali Marekani kwa kujaribu kuingilia miamala ya kibiashara baina ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyingine huru duniani.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatano katika mkutano wa Baraza la Mawaziri na kubainisha kuwa: Wamarekani wanataka kuingilia hata biashara halali ya kawaida ya mafuta baina ya mataifa mawili rafiki ambayo haiwahusu."

Amesema Washington inajaribu kutia pua katika biashara ya mafuta baina ya Iran na Venezuela katika hali ambayo, uingiliaji huo hauna msingi wowote wa kisheria.

Kauli ya Dakta Rouhani inajiri wakati huu ambapo tayari meli tatu za mafuta za Iran kati ya tano zimeshatia nanga nchini Venezuela.

Wananchi wa Venezuela wakishangilia kuwasili nchini humo meli za mafuta za Iran

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, bila ushirikiano baina ya mihimili ya dola na majeshi ya Iran, Marekani ingetekeleza uvamizi dhidi ya meli hizo za mafuta za Iran, kama tukio la mwaka jana 2019 la kusimamishwa meli ya mafuta ya Iran katika eneo la Jabal Tur (Gibraltar).

Meli tatu za mafuta za Iran zimewasili nchini Venezuela licha ya makelele na vitisho vya Marekani vya kutaka kuzisimamisha na hata kuzishambulia.

Tags