Mohammad Bagher Ghalibaf achaguliwa kuwa Spika mpya Bunge la Iran
Mohammad Bagher Ghalibaf ndiye spika mpya wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran. Zoezi la kumchagua spika wa bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu limefanyika leo asubuhi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, wabunge wa bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo asubuhi wamefanya kikao cha wazi na kumchagua Mohammad Bagher Ghalibaf kuwa spika mpya kwa kura 230 za ndio kati ya kura zote 264.
Sayyid Mostafa Agha Mirsalim na Fereidoun Abbasi ambao walishiriki katika mchuano huo wamepata kura 12 na 17 kwa utaratibu.
Kikao hicho cha bunge la Iran kimewachagua pia Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi na Ali Nikzad kuwa Manaibu Spika wa Kwanza na wa Pili wa bunge hilo la 11 la Jamhuri ya Kiislamu.
Uchaguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulifanyika tarehe 21 Februari mwaka huu kwa ajili ya kuchagua wabunge 290 katika majimbo 208 ya uchaguzi kote nchini Iran. Zaidi ya watu milioni 24 na laki tano waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki kwenye uchaguzi huo.
Kati ya majimbo hayo 208, wabunge wa majimbo 197 walipatikana katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo na uchaguzi wa majimbo 11 tu ndio ulioingia katika duru ya pili ambayo inatarajiwa kufanyika tarehe 11 Septemba mwaka huu.