Waliopona COVID-19 nchini Iran wapindukia 112,000
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathirika 112,998 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran ametangaza hayo leo Alkhamisi katika kikao cha kila siku na waandishi habari na kuongezka kuwa wagonjwa wapya 2,258 wa COVID-19 wamegundulika Iran katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Jahanpour ameongeza kuwa kwa ujumla watu walioambukizwa COVID-19 nchini Iran ni 143, 849.

Daktari Jahanpur hali kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 63 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo mchana na kusema kuwa, hadi sasa watu 7,627 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.
Idadi jumla ya walioambukizwa COVID-19 duniani hadi kufikia sasa ni milioni 5.8 na waliopoteza maisha ni zaidi ya 357,000. Marekani inaongoza duniani kwa maambukizi na vifo vya corona ambapo hadi kufikia leo watu milioni 1.74 walikuwa wameambukizwa COVID-19 na wengine zaidi ya laki moja wamepoteza maisha.