"Hatukuiruhusu Marekani ikandamize kwa goti uzalishaji nchini Iran"
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kaulimbiu ya 'Ustawi mkubwa katika Uzalishaji' ndiyo suluhu ya matatizo yote ya kiuchumi ya Jamhuri ya Kiislamu, na hilo litaafikiwa kwa ushirikiano na jitihada za pamoja.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatatu hapa Tehran na kusisitiza kuwa, ushirikiano wa wananchi wa Iran umelipa taifa hili matumaini ya kuwa na mustakabali mzuri mbali na kutoa pigo kwa maadui.
Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, "taifa hili halikuiruhusu Marekani iukandamize kwa goti uzalishaji nchini Iran chini ya kaulimbiu ya Ustawi mkubwa katika Uzalishaji. Hili limewakera maadui wanaofanya jitihada za kuwakatisha tamaa Wairani na kuwaonyesha kuwa serikali yako imefeli katika utendajikazi."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliutaja mwaka huu wa 1399 Hijria Shamsia ulioanza Machi 20 nchini Iran kuwa ni Mwaka wa Ustawi Mkubwa katika Uzalishaji.
Itakumbukwa kuwa, mnamo Mei 25, afisa wa polisi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesta nchini Marekani alimbinya shingo kwa kutumia goti kwa dakika 9 hivi George Floyd, Mmarekani mweusi mwenye asili ya Afrika hadi akakata roho.
Muaji hayo ya kikatili chini ya kaulimbiu ya "Siwezi kupumua" matamshi yaliyosikika yakitoka kinyonge kinywani mwa Floyd alipokuwa akiuawa, yanaendelea kushuhudiwa ndani na nje ya Marekani.