Rouhani: Marekani inapanga njama kuzuia kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kufutwa vikwazo vyote vya silaha dhidi ya Iran baadaye mwezi Oktoba mwaka huu na kusema Marekani imeghadhabishwa na mpango wa kufutwa vikwazo hivyo na sasa inapanga njama ya kutaka vikwazo hivyo visalie.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo Jumatano katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kusistiza kuhusu ulazima wa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusimama kidete mbele ya njama hiyo ya Marekani.
Rais Rouhani amesema Iran inatarajia kuwa wanachama wa Baraza la Usalama watasimama kidete mbele ya njama za Marekani kwa ajili ya uthabiti wa kimataifa ambao ulikusudiwa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA.
Rais Rouhani ameashiria kufeli njama za Marekani dhidi ya Iran na kusema: Wamarekani wafahamu kuwa, iwapo wanalenga kukiuka azimio 2231 na kisha watayarishe azimio jipya dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo wa kujilinda katika hali yoyote ile.

Amekumbusha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliweza kuunda mfumo bora zaidi wa kujihami angani wakati ikiwa inakabiliwa na vikwazo na ikafanikiwa kutungua drone vamizi ya Marekani.
Aidha amesema sera za mashinikizo ni sera za daima za Marekani ambayo inataka kujifanya kuwa polisi ya dunia.
Rais wa Iran amebaini kuwa, kukabiliana Iran na corona na vikwazo vilivyo kinyume cha sheria vya Marekani ni jambo ambalo litabakia katika historia. Ameongeza kuwa, taifa la Iran kwa umoja na mshikamano wa kitaifa litasambaratisha njama zote za Marekani.