Iran yapinga madai ya UN kuwa 'makombora yaliyotoka Iran' yalilenga Saudia
Iran imepinga madai ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuwa makombora yaliyotumiwa kushambulia Saudia 'yalitoka Iran' na kusema umoja huo umetoa tamko hilo chini ya mashinikizo ya Marekani na utawala wa Saudia.
Katika taarifa siku ya Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imebainisha wasi wasi wake kuhusu Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kutumiwa kufikia malengo ya kisiasa.
Taarifa hiyo imesema kutayarisha ripoti kwa madhumini ya kisiasa hakutabadilisha ukweli na kwamba hali ya mambo Asia Magharibi inatokana na sera potovu za Marekani na utawala wa Saudia unaowaua watoto.
Siku ya Alhamisi katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwasilisha ripoti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu makombora ya cruise yaliyotumiwa kushambulia vituo vya mafuta na uwanja wa kimataifa wa ndege Saudia Novemba 2019 na Februari 2020 na kusema makombora hayo "yalitoka Iran."
Aidha amesema, 'kuna uwezekano zana hizo zilisafirishwa kinyume cha azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo liliidhinisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA, yaliyotiwa saini baina ya Iran na madola makubwa duniani mwaka 2015."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetaka Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa yasiingizwe katika mtego wa Marekani wa kutaka Iran isiondolewe vikwazo.
Wakati huo huo Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa Majid Takhte-Ravanchi amesema Iran inapinga ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa. Amesema Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hayana utaalamu wala ujuzi unaohitajika kufanya utafiti. Takhte-Ravanchi amesema Marekani ina uhasama na Iran na hivyo haiwezi kuwa ni yenye kutathmini masuala ya Iran katika Umoja wa Mataifa.