Rabiei: Iran ina mpango wa nyuklia uliowazi zaidi duniani
Msemaji wa Serikali ya Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu ndio nchi pekee duniani ambayo imeupa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) idhini ya kutembelea vituo vyake vya nyuklia mara nyingi zaidi. Aidha ameongeza kuwa: "Mpango wa nyuklia wa Iran ni wenye uwazi zaidi duniani."
Ali Rabiei Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo Jumanne katika mkutano na waandishi habari na kuongeza kuwa, Iran inataraji Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki utawasilisha maombi yake kwa mujibu wa kanuni za wakala huo. Ameongeza kuwa, kutumia vigezo vya kisiasa katika kazi za IAEA hakutakuwa na natija nyingine ghairi ya kuvuruga uthabiti wa dunia.
Aidha amesema Wanachama wa Bodi ya Magavana wa IAEA wanapaswa kulinda uhuru wa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa mkabala wa utumiaji mabavu wa Marekani.

Rabiei amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafungamana na ahadi zake zote za kimataifa na thibitisho la hilo ni ripoti 17 za IAEA ambazo zimeonyesha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran unafanyika kwa malengo ya amani.
Msemaji wa Serikali ya Iran aidha amelaani njama za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki dhidi ya Iran. Amesema mataifa ya dunia yanafahamu kuhusu chokochoko za Marekani na uchochezi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran na hivyo Marekani inapaswa kusikiliza sauti ya jamii ya kimataifa na isitishe ubabe wake dhidi ya mataifa mengine.