Mousavi: Marekani na Saudia zinadhihaki mfumo wa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61660-mousavi_marekani_na_saudia_zinadhihaki_mfumo_wa_kimataifa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali namna Umoja wa Mataifa unavyoshawishiwa vibaya na kusema: "Saudi Arabia kwa kutumia pesa na Marekani kwa kutumia ubabe, kwa pamoja zinaudhihaki mfumo wa kimataifa."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2020 06:37 UTC
  • Mousavi: Marekani na Saudia zinadhihaki mfumo wa kimataifa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali namna Umoja wa Mataifa unavyoshawishiwa vibaya na kusema: "Saudi Arabia kwa kutumia pesa na Marekani kwa kutumia ubabe, kwa pamoja zinaudhihaki mfumo wa kimataifa."

Sayyid Abbas Mousavi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo Jumatano ya leo katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake binafsi wa Twitter na kuongeza kuwa: "Siku kadhaa baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran, amefumbia macho vitendo vya muungano wa kivita wa Saudia nchini Yemen na ameyafanya hayo pamoja na kuwa amekubali kuwa muungano huo umeuua mamia ya watoto wa Yemen."

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu alitangaza kuuondoa muungano wa kivita wa Saudia dhidi ya Yemen katika orodha ya fedheha ya umoja huo ambayo huorodhesha makundi au nchi zinazoua na kukiuka haki za watoto.

Watoto ni waathirika wakuu wa mashambulizi ya muungano wa kivita wa Saudia dhidi ya Yemen

Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa uliiweka Saudia katika orodha hiyo ya fedheha kutokana na mashambulizi yake ya Yemen ambayo yalipelekea tatoto zaidi ya 683 kuuawa na kujeruhiwa wakati huo. Aidha Saudia iliwekwa katika orodha hiyo kutokana na hatua yake ya kudondosha mabomu ambayo hulenga shule na hospitali za Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya ya Yemen, tokea muungano  huo uanzishe hujuma dhidi ya Yemen mwezi Macho 2015 hadi sasa watoto 7,732 wa Yemen wameuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi ya muungano huo hasimu huku watoto wengine milioni mbili na nusu wakiwa wanakabiliwa na lishe duni.