Iran yafanyia majaribio makombora mapya ya cruise
Jeshi la Baharini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limefanyia majaribio kwa mafanikio makombora yake mapya ya cruise katika luteka ya kijeshi iliyofanyika kaskazini mwa Bahari ya Hindi na katika Bahari ya Oman.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRNA, Jeshi la Majini la Iran limevurumisha makombora ya masafa mafupi na yale ya masafa marefu katika mazoezi hayo ya kijeshi.
Makombora ya masafa marefu ya kizazi kipya yamelenga shabaha kwa mafanikio makubwa hadi umbali wa kilomita 280.
Katika maneva hiyo ya kijeshi ya jana Alkhamisi, makombora ya ardhini hadi baharini na baharini hadi baharini ya Iran ya Kiislamu yamelenga shabaha kwa usahihi mkubwa.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya ulinzi huku ikijitosheleza kwa kiasi kikubwa katika zana za kujihami. Jeshi la Iran hufanya mazoezi ya mara kwa mara kwa ajili ya kuonyesha uwezo wa vikosi vyake na pia kufanyia majaribio zana mpya za kivita.
Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa, uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi zingine bali sera yake ya ulinzi imejengeka katika msingi wa kujihami.