Mousavi: Troika ya Ulaya haina mwamana hata chembe
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia vitendo vya kindumilakuwili vya nchi tatu za Ulaya yaani Troika ya Ulaya zilizomo kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA ambazo ni Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na kusema kuwa, kitendo cha nchi hizo cha kuishinikiza Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kutoa azimio la kisiasa dhidi ya Iran hakikubaliki kabisa.
Sayyid Abbas Mousavi amesema leo hayo alipohojiwa na shirika la habarila IRIB na kuongeza kuwa, kinachopelekea kitendo hicho cha bodi ya magavana kutokubalika ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi yenye ushirikiano wa kiwango cha juu zaidi na cha wazi zaidi na wakala wa IAEA na hata wakala huo pia umekiri mara chungu nzima suala hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezilaumu nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa kwa vitendo vyao vya nyuso mbili na vya kustaajabisha na kusema kwa kusisitiza kuwa, kwa mara nyingine, nchi hizo zimelifanya taifa la Iran lisiwe na imani nao kabisa.
Vile vile amezionya nchi hizo za Ulaya pamoja na Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki IAEA kutofuata siasa ghalati akisema, matokeo mabaya ya kutolewa azimio la kisiasa dhidi ya mradi wa amani wa nyuklia wa Iran, bila ya shaka yoyote yatawarejea watu wale wale walioandaa na kushinikiza kutolewa azimio hilo.
Aidha amesema serikali na taifa la Iran halitosalimu amri mbele ya mashinikizo na siasa za kupenda makubwa za mabeberu wa dunia na kuongeza kuwa, wajumbe wa Bodi ya Magavana ya IAEA wanapaswa kuwa macho mbele ya njama za Marekani na utawala wa Kizayuni za kufufua kesi ya zamani na bandia.