Kamanda Dehqan: Chokochoko za Marekani dhidi ya Iran zitapata jibu kali
Mshauri wa Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran katika masuala ya sekta ya viwanda vya ulinzi amesisitiza kuwa, chokochoko zoazote za Marekani dhidi ya Iran katika maji ya Ghuba ya Uajemi zitapata majibu makali kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Brigedia Jenerali Hossein Dehqan amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya al Jazeera na huku akibainisha kwamba rais wa Marekani, Donald Trump ni mhalifu na si rais wa nchi amesema, kamwe Iran haiwezi kufanya mazungumzo yoyote yale na Trump.
Aidha amesema, kamwe Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitofanya mazungumzo ya kujadili nguvu zake za makombora wala siasa zake katika eneo hili.
Mshauri huyo wa Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran katika masuala ya sekta ya viwanda vya ulinzi vile vile amesema kuhusu matukio ya kisiasa na kiusalama ya Yemen kwamba, fujo ndizo zilizotawala nchini Yemen hivi sasa na hayo ndiyo matunda ya uvamizi wa Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo.
Amesema, mwarubaini wa mgogoro wa Yemen ni Saudia kukiri kuwa imeshindwa katika vita vya kivamizi ilivyovianzisha nchini humo na ibadilishe siasa zake kuhusu Yemen. Amma kuhusiana na uwezekano wa kufanyika mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia, Brigedia Jenerali Dehqan amesema, Tehran haina tatizo katika jambo hilo, lililo muhimu ni Saudia tu irekebishe siasa zake na ibadilishe misimamo yake kuhusu Iran.
Kuhusu matukio ya Libya, mshauri huyo wa Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran katika masuala ya sekta ya viwanda vya ulinzi amesema, Iran inaitambua Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya kwani ndiyo inayotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa.