Iran, kinara wa mapambano dhidi ya mihadarati duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61792-iran_kinara_wa_mapambano_dhidi_ya_mihadarati_duniani
Mwakilishi wa Ofisi ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Jinai ya Umoja wa Mataifa mjini Tehran, Alexander Fedulov, ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jitihada zake kubwa za kupambana na dawa za kulevya. Fedulov ameyasema hayo katika kikao cha wataalamu kilichofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Mihadarati kilichofanyika kwa njia ya video.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2020 06:10 UTC
  • Iran, kinara wa mapambano dhidi ya mihadarati duniani

Mwakilishi wa Ofisi ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Jinai ya Umoja wa Mataifa mjini Tehran, Alexander Fedulov, ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jitihada zake kubwa za kupambana na dawa za kulevya. Fedulov ameyasema hayo katika kikao cha wataalamu kilichofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Mihadarati kilichofanyika kwa njia ya video.

Uraibu wa dawa za kulevya ni tishio kwa dunia nzima kama yalivyo maradhi ya COVID-19 na virusi vya corona, na unahitajia azma kubwa na mapambano makali na ya muda mrefu. Pamoja na hayo hatupasi kufumbia macho sababu na chanzo za matatizo na changamoto nyingi zinazoikabili jamii ya mwanadamu likiwemo tatizo la mihadarati na dawa za kulevya. 

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, uzembe wa jamii ya kimataifa na kutotilia maanani suala la kilimo na uzalishaji wa dawa kulevya katika maeneo mbalimbali ya dunia ikiwemo Afghanistan ambayo ndiyo kituo kikuu cha kilimo cha mpopi na uzalishaji wa afyuni, kumepelekea kushuhudiwa ongezeko katika uzalishaji wa dawa hizo mwaka uliopita wa 2019.

Kilimo cha mpopi na uzalishaji wa mihadarati umeongezeka huko Afghanistn licha ya kuwepo maelfu ya wanajeshi wa Marekani nhini humo.

Taarifa za Idara ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, ongezeko la magendo ya dawa za kulevya linasababisha vifo vya karibu watu laki moja kwa mwaka. Vilevile biashara ya magendo ya dawa za kulevya inaimarisha uwezo wa kifedha wa makundi ya kigaidi na kustawisha zaidi mitandao ya makundi yenye mitazo na fikra za kuchupa mipaka; jambo ambalo pia linatishia usalama na amani ya kimataifa. Katika mazingira kama haya hapana shaka kuwa, njia pekee na muhimu zaidi ya kukabiliana na uzalishaji na magendo ya dawa za kulevya na mihadarati ni kuimarisha jitihada za jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo.

Hivi sasa ambapo imepita karibu miaka 19 ya kuwepo majeshi ya Marekani katika ardhi ya Afghanistan takwimu zinaonyeswa kuwa, kilimo cha mpopi na uzalishaji wa afyuni umeongezeka mara kadhaa nchini humo ikilinganishwa na mwaka 2001 ambao unatajwa kuwa eti ni mwaka wa kuanza mapambano ya Marekani dhidi ya ugaidi na mihadarati. Takwimu hizo zinasema kuwa, uzalishaji wa dawa za kulevya nchini Afghanistan umeongezeka na kufikia tani 4,800 kwa mwaka.

Askari wa Marekani katika mashamba ya mihadarati, Afghanistan

Katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mihadarati na dawa na kulevya. Haya yanathibitishwa na takwimu na ripoti mbalimbali zinazotolewa na taasisi za kimataifa. Ripoti ya mwaka huu ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa: Asilimia 90 ya afyuni, asilimia 26 ya heroini na asilimia 28 ya morfini yote iliyokamatwa katika upeo wa dunia nzima iligunduliwa na kukamatwa nchini Iran ikiwa njiani kutoka Afghanistan kuelekea katika maeneo mbalimbali ya dunia. Kugunduliwa zaidi ya tani 950 za aina mbalimbali za mihadarati hapa nchini katika kipindi cha mwaka mmoja tu ambayo ilikuwa ikisafirishwa kupelekwa katika nchi nyingine, kunatambuliwa kuwa ni mafanikio muhimu na huduma kubwa kwa jamii ya mwanadamu.

Vita dhidi ya mihadarati nchini Iran

Mapambano hayo makubwa ya Iran dhidi ya mihadarati yameiwezesha kutunukiwa nishani 8 za Idara ya ya Kupambana na Mihadarati ya Umoja wa Mataifa. Itakumbukwa pia kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza mashujaa karibu elfu nne waliouawa shahidi wakipambana na magenge ya kusafirisha dawa za kulevya kupitia kwenye mipaka na ardhi yake na kuelekea katika maeneo mengine ya dunia. Kwa mnasaba huo pia mwakilishi wa Idara ya Kupambana na Mihadarati na Jinai ya Umoja wa Mataifa mjini Tehran, Alexander Fedulov amesema: Jitihada kubwa za Jamhuri ya Kiislamu katika kukabiliana na kupambana na changamoto ya kimataifa ya dawa za kulevya zinapaswa kupongezwa. Fedulov amesema kuwa: Umoja wa Mataifa unafanya kila linalowezekana kwa ajili ya kustawisha zaidi kiwango cha ushirikiano na kubadilishana mawazo na Iran kuhusiana na suala la kupambana na mihadarati.

Hapana shaka kuwa, mapambano dhidi ya mihadarati yana maslahi na manufaa kwa nchi nyingi hususan zile za Ulaya. Pamoja na hayo inasikitisha kwamba, nchi hizo za Ulaya zinakataa kusaidia jitihada za Iran za kupambana na magenge ya dawa za kulevya kutoka Afghanistan na nchi nyingiene jirani au hata kuiuzia zana zinazohitajika kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya janga hilo la kimataifa.