"Marekani kuikingia kifua Israel kumelishushia hadhi Baraza la Usalama"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61808-marekani_kuikingia_kifua_israel_kumelishushia_hadhi_baraza_la_usalama
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema hatua ya Marekani ya kuendelea kuukingia kifua na kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel imelifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lipoteze hadhi yake na likose maana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2020 03:19 UTC

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema hatua ya Marekani ya kuendelea kuukingia kifua na kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel imelifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lipoteze hadhi yake na likose maana.

Majid Takht-Ravanchi aliyasema hayo jana Jumatano katika mkutano wa Baraza la Usalama kwa njia ya inteneti wa kujadili kadhia ya Palestina ambapo ameongeza kuwa, kitendo cha Washington cha kuendelea kuunga mkono sera za mabavu za utawala haramu wa Israel na zilizo kinyume cha sheria ndani ya miongo saba iliyopita, kimeupa jeuri utawala huo wa kuendelea kukanyaga sheria za msingi za kimataifa na kufanya jinai za kutisha ukijua kuwa hautawajibishwa.

Amesema, "mfano hai wa jinai hizo ni kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kuendeleza mzingiro usio wa kibinadamu dhidi ya Ukanda wa Gaza, na kuendelea kwa mpangilio maalumu ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala Syria na Lebanon, kinyume kabisa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa."

Benjami Netanyahu (kulia) na Donald Trump

Mwandiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, tabia ya Marekani ya kuendelea kutumia vibaya nafasi yake kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, imeikingia kifua Israel na kulifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lisiweze kuuwajibisha utawala huo pandikizi kwa jinai zake.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, kwa kutekeleza mpango wake wa kupora na kuunganisha maeneo muhimu ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine ya Palestina unaoyakaliwa kwa mabavu, utawala huo ghasibu utakuwa umefungua ukurasa mpya katika muendelezo wake wa dhulma na jinai.