Mousavi: Wairani ni wahanga wa magaidi wanaosaidiwa na kufadhiliwa na Marekani
-
Sayyid Abbas Mousavi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amejibu tuhuma na madai yasio na msingi yaliyotolewa na Marekani dhidi ya Iran akisema utawala wa Marekani ambao ndio mfadhili mkuu wa ugaidi wa kiserikali duniani hauna hadhi ya kutoa madai ya kupambana na ugaidi au kutoa hukumu na maamuzi katika uwanja huu.
Sayyid Abbas Mousavi amejibu ripoti ya kila mwaka ya Marekani kuhusiana na ugaidi akisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga na kulaani ripoti hiyo kwa sababu ya uzushi wake, kutokuwa na ukweli na vigezo vya kindumakuwili vya utawala wa Marekani katika kupambana na ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Marekani ambayo inatambulika kama mfadhili mkuu wa ugaidi wa kiserikali na muungaji mkono mkuu wa utawala vamizi na wa Kizayuni wa Israel, haina sifa na hadhi ya kutoa madai ya kupambana na ugaidi.
Mousavi amesema kuwa, historia ya miongo kadhaa ya karibuni inaonyesha waziwazi kwamba, Marekani ilihusika katika kuanzisha makundi ya kigaidi kama wanavyokiri baadhi ya wanasiasa wa nchi hiyo na inaendelea kuyafadhili na kuyasaidia makundi hayo. Ameongeza kuwa, Donald Trump mwenyewe alikili katika kampeni zake za uchaguzi kwamba, serikali za kabla yake ndizo zilizoanzisha kundi la kigaidi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi.
Katika ripoti yake ya kila mwaka kuhusu ugaidi iliyotolewa Jumatano ya wiki hii, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani, kama ilivyo kawaida ya kila mwaka, iliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaunga mkono ugaidi.