Iran: Aziomio lililopendekezwa na Marekani ni haribifu kwa Baraza la Usalama
Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema rasimu ya azimio ambalo limependekezwa na Marekani kwa ajili ya kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ni kinyume cha azimio 2231 na ni kosa kubwa ambalo litakuwa haribifu kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Majid Takhte-Ravanchi Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amongeza kuwa azimio hilo ambalo limependekezwa na Marekani linapaswa kupingwa.
Aidha mwanadiplomasia huyo wa Iran amesisitiza kuwa, Russia na China kama wanachama wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wenye kura ya turufu wanaunga mkono mapatano ya nyuklia ya JCPOA sambamba na utekelezwaji kamili wa azimio 2231. Amesema hatua ya Marekani ya kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran itakuwa na matokeo mabaya kwa sheria za kimataifa na ushirikiano na Baraza la Usalama.
Siku ya Jumatano, Kelly Craft, mwakilishi wa kudumua wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na Brian Hook mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran walikariri madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na kujaribi kuwakinaisha wajumbe wa Baraza la Usalama warefushe vikwazo dhidi ya Iran.

Marekani imeanzisha kampeni kubwa za kimataifa za kulizuia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lisitekeleze azimio lake nambari 2231 linalotoa amri ya kuiondolea Iran vikwazo vya silaha ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu wa 2020. Marekani inaendesha njama hizo kama sehemu ya kukabiliana na uwezo mkubwa wa kiulinzi na kijeshi wa Iran unaozidi kukua na kuwa imara siku baada ya siku.