Faili la kuuawa Qassim Soleimani: Iran yatoa waranti wa kutiwa mbaroni Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61910-faili_la_kuuawa_qassim_soleimani_iran_yatoa_waranti_wa_kutiwa_mbaroni_trump
Mwendesha Mashtaka wa Tehran ametoa waranti wa kutiwa mbaroni watu 36 akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani wakihusishwa na mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) Luteni Jenerali Shahid Qassem Soleimani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 30, 2020 03:46 UTC
  • Donald Trump
    Donald Trump

Mwendesha Mashtaka wa Tehran ametoa waranti wa kutiwa mbaroni watu 36 akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani wakihusishwa na mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) Luteni Jenerali Shahid Qassem Soleimani.

Akizungumza katika kikao cha Baraza Kuu la Mahakama Iran, Ali Alqasi-Mehr, Mwendesha Mashtaka wa Tehran ameashiria hatua zilizochukuliwa na Iran katika kufuatilia faili na mauaji ya Luteni Jenerali Qassim Soleimani na kusema kuwa, watu waliohusika, kushiriki na kusaidia mauaji dhidi ya kamanda huyo wameshafahamika.

Amesema kuwa, waliohusika na mauaji hayo wamo wanasiasa, maafisa wa kijeshi wa Marekani na wa nchi nyingine akiwemop Rais Donald Trump ambao wote wanapaswa kukamatwa kwa mujibu wa waranti iliyotolewa. 

Mwendesha Mashtaka wa Tehran  ameeleza kuuwa, tayari wameitaka Polisi ya Kimataifa Interpol kuwatia mbaroni watu hao.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani

Aidha ameongeza kuwa, Rais Trump atafuatiliwa kisheria hata baada ya kumaliza muhula wake wa urais nchini Marekani.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 3 Januari mwaka huu, jeshi la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump lilimuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani akiwa uraiani nchini Iraq tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Baghdad. Viongozi wa Iraq walisema, walikuwa wamemwalika Luteni Jenerali Qassem Soleimani aende nchini humo kufuatilia juhudi za Baghdad za kuzipatanisha nchi mbili za Iran na Saudi Arabia.

Nchi nyingi duniani, mashirika, taasisi na makundi mbalimbali yalilaani vikali mauaji hayo ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya kamanda huyo shujaa aliyekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi.